Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri Mkuu amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anawapa pole waathirika wote na kusisitiza dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwasaidia. “Ujenzi huu ni ishara ya upendo na kujali kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, aliyetoa maelekezo ya kujenga nyumba bora na za kudumu kwa waathirika waliopoteza makazi yao,” alisema.
Katika ujenzi huo, nyumba 73 kati ya 109 zimejengwa na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA-JKT) kwa gharama za Serikali Kuu, nyumba 35 zimejengwa na Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania, na moja imejengwa na Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (UWT).
Waziri Mkuu aliongeza kuwa Rais Dkt. Samia alitoa shilingi bilioni 1.38 kwa ajili ya kuweka huduma za kijamii kama umeme, maji, na barabara za kuaminika ili kuhakikisha kila nyumba inafikiwa na huduma hizo. “Lengo ni kujenga makazi salama na yenye huduma muhimu za kijamii kwa waathirika wetu,” alisisitiza.
Aidha, Waziri Mkuu ameagiza Halmashauri ya Wilaya ya Hanang kuratibu ugawaji wa viwanja vya ziada katika eneo hilo kwa maendeleo zaidi. “Tunataka eneo hili lisitambulike kama makazi ya waathirika pekee, bali liwe kijiji rasmi chenye huduma zote muhimu na mfano wa maboresho ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi,” alisema.
Mapema, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi alimshukuru Rais Dkt. Samia kwa maono na miongozo yake thabiti katika kushughulikia athari za maafa hayo. Alieleza kuwa, mbali na nyumba, Rais Samia pia alitoa majiko ya gesi 109 kwa wakazi wa eneo hilo, hatua inayolenga kuboresha maisha yao kwa ujumla.
Matokeo ChanyA+ Chombo kinachounga mkono matokeo yote chanyA+ TanzaniA+. #InfoChanyA+