VIJANA WAMWAGA SIFA KWA SERIKALI KATIKA KONGAMANO LA KUPINGA DAWA ZA KULEVYA JIJINI DODOMA

Katika kilele cha Kongamano la Vijana Kupinga Matumizi na Biashara ya Dawa za Kulevya lililoandaliwa na Mamlaka ya Kupiga vita na Kupambana na dawa za kulevya (DCEA) lililofanyika katika Ukumbi wa Generali Mabeyo jijini Dodoma, vijana kutoka maeneo mbalimbali ya nchi walijitokeza kwa wingi kuunga mkono juhudi za serikali katika kupambana na janga la dawa za kulevya. Kongamano hilo, lililofanyika kwa lengo la kutoa elimu, kuhamasisha mabadiliko chanya na kushirikisha vijana kama mawakala wa mabadiliko, lilikuwa na shamrashamra za hotuba, burudani, ushuhuda wa waliowahi kuwa waraibu, na maonesho ya kazi za vijana waliopata ujuzi kupitia programu za serikali.

Vijana walioshiriki waliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua madhubuti ilizochukua kudhibiti uingizaji na usambazaji wa dawa za kulevya nchini. Walisema kuwa juhudi hizo zimeokoa maisha ya maelfu ya vijana na kuwapatia matumaini mapya.

Aidha, walieleza kufurahishwa na uwepo wa huduma za tiba kwa waraibu kupitia vituo vya afya vya serikali na mashirika binafsi, sambamba na fursa walizopata za mafunzo ya ujuzi stadi katika vyuo mbalimbali kama VETA na taasisi za kijamii. Mafunzo hayo yamewawezesha vijana kujiajiri na kujitegemea, hivyo kujiepusha na vishawishi vya dawa za kulevya.

Wakati wa tamasha hilo, vijana walisisitiza kuwa elimu, msaada wa kitabibu na fursa za kiuchumi ni nguzo kuu za vita dhidi ya dawa za kulevya. Walitoa rai kwa serikali na wadau kuendelea kushirikiana katika mapambano haya kwa kutumia sanaa, michezo, na mafunzo kwa vijana kama silaha madhubuti za kuokoa kizazi cha leo na kesho.

Alhamisi, 26 Juni, ni kilele cha maadhimisho ya kupiga vita matumizi na biashara ya dawa za kulevya, ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete – Dodoma.

Kauli mbiu: “Wekeza kwenye Kinga na Tiba dhidi ya dawa za kulevya”

Mwisho.

Unaweza kuangalia pia

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na viongozi mbalimbali kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Maafisa na Askari wa Kikosi Kazi kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) walioshiriki Ujenzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa (MMUT), Kikombo Mkoani Dodoma

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *