Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa sasa inashirikiana kwa karibu na asasi mbalimbali za kiraia katika kutoa elimu ya madhara ya dawa za kulevya kwa jamii. Ushirikiano huu unalenga kuimarisha uhamasishaji, kuibua taarifa kutoka kwa wananchi, na kushirikiana katika kutoa msaada kwa waathirika. Kupitia mikutano ya kijamii, semina, na kampeni za uelimishaji, DCEA na asasi hizo zinafikia makundi mbalimbali, hasa vijana, ili kuwakinga dhidi ya matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Ushirikiano huu ni nguzo muhimu katika kuimarisha mapambano haya kwa njia shirikishi.
Pia, DCEA inaonyesha kwa uwazi aina mbalimbali za dawa za kulevya kama bangi, heroin, cocaine, mirungi, na dawa za hospitali zinazotumika vibaya. Hii inawawezesha wananchi kuzijua kwa macho na kuwa na uelewa wa namna zinavyoonekana, jambo ambalo linawasaidia kutoa taarifa sahihi na kwa wakati wanapoziona katika maeneo yao.
Uelewa huu pia huongeza ushirikishwaji wa jamii katika mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya dawa hizo, hivyo kusaidia kuokoa maisha ya vijana na kulinda amani na ustawi wa taifa kwa ujumla.
Alhamisi, 26 Juni, ni kilele cha maadhimisho ya kupiga vita matumizi na biashara ya dawa za kulevya, ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete – Dodoma. Kauli mbiu:
“Wekeza kwenye Kinga na Tiba dhidi ya dawa za kulevya”
Mwisho.
Matokeo ChanyA+ Chombo kinachounga mkono matokeo yote chanyA+ TanzaniA+. #InfoChanyA+