Mara baada ya kufungwa kwa mashindano mbalimbali yaliyoandaliwa katika kuadhimisha Wiki ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya Duniani, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini Tanzania, Aretas Lyimo, amesema kuwa Tanzania imeonesha dhamira ya kweli kwa vitendo katika mapambano hayo kwa kushirikisha jamii, hususan vijana, katika michezo na elimu ya kupinga matumizi na biashara ya dawa hizo.
Amesema kuwa katika kipindi cha wiki mbili, Tanzania imeandaa mashindano na matukio mbalimbali ya kijamii yaliyolenga kutoa elimu na kuhamasisha vita dhidi ya dawa za kulevya. Mashindano hayo yamehusisha michezo ya kukimbiza kuku, kukimbia na magunia, kucheza rede, pamoja na mpira wa miguu ulioshirikisha timu nane kutoka maeneo mbalimbali ya Dodoma.
Katika fainali ya mpira wa miguu iliyofanyika kwenye Viwanja vya Chuo Kikuu cha Mtakatifu John, timu ya Wagoloko FC iliibuka kidedea kwa kuifunga Mwaise FC mabao 2–0, mbele ya mamia ya mashabiki waliokuwa wakishangilia kwa hamasa kubwa. Kamishna Lyimo amesema tukio hilo limekuwa zaidi ya mchezo; limekuwa darasa la mshikamano, nidhamu na mapambano ya pamoja dhidi ya dawa za kulevya.
“Vijana wamejitokeza kwa wingi sana kushiriki si tu kwenye mashindano, bali pia kusikiliza elimu ya athari za dawa za kulevya. Hili linaonesha kwamba jamii inazidi kufunguka na kuunga mkono jitihada za serikali,” alisema Lyimo kwa furaha.
Aidha, alieleza kuwa wiki hii ya maadhimisho imeonesha mafanikio makubwa katika kuwafikia vijana kwa njia rafiki na jumuishi, na kwamba Tanzania imeidhihirishia dunia kuwa inapambana kwa nguvu zote dhidi ya dawa za kulevya. Akasisitiza kuwa ushirikiano kati ya serikali, jamii na taasisi mbalimbali ni silaha muhimu katika vita hii.
Katika kuendeleza maadhimisho hayo, Kamishna Lyimo alieleza kuwa kuna matukio mengine muhimu yaliyopangwa kuelekea kilele cha Siku ya Kupiga Vita Matumizi na Biashara ya Dawa za Kulevya ifikapo tarehe 26 Juni 2025, ambapo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Wiki ya maadhimisho ya Kupiga Vita Matumizi na Biashara ya Dawa za Kulevya imeambatana na matukio mbalimbali muhimu. Mnamo Jumatatu, 23 Juni 2025, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) itafanya ziara kwenye vyombo vya habari kuhamasisha jamii, huku Mhe. William Lukuvi akitoa taarifa rasmi Bungeni kuhusu hali ya dawa hizo nchini.
Jumanne, 24 Juni, kutakuwa na Kongamano la Vijana litakaloongozwa na Dkt. Dorothy Gwajima, likifuatiwa na ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Senyamule, kwenye mabanda ya maonesho.
Jumatano, 25 Juni, Mhe. Lukuvi ataongoza matembezi ya hamasa na kutembelea mabanda ya wajasiriamali katika Viwanja vya Jakaya Kikwete.
Alhamisi, 26 Juni, ni kilele cha maadhimisho, ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete.
Kauli mbiu: “Wekeza kwenye Kinga na Tiba dhidi ya dawa za kulevya”
Maadhimisho haya yanaonesha dhamira ya Tanzania kupambana na dawa za kulevya kwa njia za kijumuishi kama michezo, elimu, na midahalo, zikiwa njia muhimu za kuwalinda vijana na jamii.
Matokeo ChanyA+ Chombo kinachounga mkono matokeo yote chanyA+ TanzaniA+. #InfoChanyA+