Mamia ya vijana kutokamaeneo mbalimabli katika mkoa wa wa Dodoma wamekusanyika katika Ukumbi wa Generali Mabeyo jijini Dodoma kushiriki Tamasha la Vijana lililolenga kutoa elimu kuhusu madhara ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
Tamasha hili lilifanyika kwa heshima ya kuadhimisha kilele cha Siku ya Kimataifa ya Kupinga Matumizi na Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya. Mgeni rasmi katika kongamano hilo alikuwa ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (Mb), akiambatana na Waziri wa Vijana na Ajira, Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb) pamoja na Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Kamishna Aretas Lyimo.
Katika hotuba yake, Dkt. Gwajima aliwataka vijana kujitambua na kujiweka mbali na matumizi ya dawa za kulevya, akisisitiza kuwa taifa linawategemea kama nguzo ya maendeleo. “Dawa za kulevya si njia ya mafanikio, ni njia ya maangamizi. Mchague uzima, mchague ndoto zenu pia mchague rafiki mzuri ambae hatakushawishi utumie dawa za kulevya,” alisema kwa msisitizo.
Kwa upande wake, Mhe. Ridhiwani Kikwete aliwahimiza vijana kutumia fursa za ajira na ujasiriamali zinazotolewa na serikali ili kuepuka vishawishi vinavyoweza kuwaingiza kwenye matumizi ya dawa hizo.
Kamishna Aretas Lyimo alieleza kuwa vijana wengi wamepatiwa elimu na huduma za tiba na ushauri kupitia vituo vya tiba kwa waraibu nchini (MAT Clinics), ikiwa ni mafanikio ya wazi ya juhudi za serikali.
Tamasha hilo liliambatana na burudani zenye ujumbe, mashindano ya vipaji na maonesho ya kazi za vijana, likiwa chachu ya mabadiliko katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini.
Alhamisi, 26 Juni, ni kilele cha maadhimisho ya kupiga vita matumizi na biashara ya dawa za kulevya, ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete – Dodoma.
Kauli mbiu: “Wekeza kwenye Kinga na Tiba dhidi ya dawa za kulevya”
Mwisho.