Baadhi ya wananchi walioshiriki kwenye michuano ya mpira wa miguu iliyokuwa ikiendelea jijini Dodoma, wameeleza kufurahishwa na hatua ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kutumia michezo kama jukwaa la kijamii kuhamasisha mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya, hasa kwa vijana.
Michuano hiyo, iliyojumuisha timu mbalimbali, ilifikia kilele chake kwa mchezo wa fainali uliovutia mamia ya mashabiki, ambapo timu ya Wagoloko FC iliibuka mshindi kwa kuifunga Mwaise FC mabao 2–0. Ushindani uliokuwa wa hali ya juu, nidhamu na ushiriki wa vijana wengi ni kiashiria cha mafanikio makubwa ya kampeni hiyo kupitia michezo.
Wananchi na wadau wa maendeleo walieleza kuwa matumizi ya dawa za kulevya kama bangi, mirungi na mengineyo yanaathiri vibaya maisha ya vijana, hususan kupunguza uwezo wao wa kufikiria kwa kina, kufanya maamuzi sahihi na hata kuharibu ndoto zao za baadaye.
Kwa kauli mbiu “Wekeza kwenye Kinga na Tiba dhidi ya dawa za kulevya”, DCEA imeonesha njia mpya na jumuishi ya kushirikisha jamii katika mapambano haya, huku michezo ikiwafanya vijana wawe na shughuli mbadala, za afya na zenye mchango chanya kwa taifa.