Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, amesema kuwa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inayoendelea kutekelezwa nchini imefanikiwa kuwafikia Watanzania 775,119 kutoka mikoa 11 hadi kufikia tarehe 24 Januari 2025. Kampeni hii inalenga kuwasaidia wananchi kupata elimu na msaada wa kisheria ili kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Kwa mujibu wa Waziri Ndumbaro, kampeni hiyo imeleta mafanikio makubwa kwa kushughulikia matatizo ya wananchi katika maeneo muhimu kama vile, Migogoro ya umiliki na matumizi ya ardhi imetatuliwa na wananchi wamepewa elimu ya kuzingatia sheria za ardhi. Wananchi wameelimishwa kuhusu haki zao za msingi na jinsi ya kuzilinda, Jamii imefundishwa umuhimu wa uwajibikaji na uadilifu katika uongozi.
Vile vile imetolewa Elimu ya kuandika na kutekeleza wosia ambayo imewasaidia wananchi kupunguza migogoro ya familia, elimu kuhusu haki na wajibu wa wanandoa imewasaidia kupunguza migogoro ya ndoa.
Hali kadhalika Kampeni imehamasisha jamii kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto, iletoa Elimu kuhusu taratibu za madai na jinai a,nbayo imewasaidia wananchi kuelewa haki zao kisheria na Mamia ya wananchi wamepatiwa msaada wa usajili wa vyeti vya kuzaliwa na vifo.
Waziri Ndumbaro amesisitiza kuwa kampeni hii ni kielelezo cha dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki bila ubaguzi. Pia amepongeza ushirikiano wa wananchi na taasisi mbalimbali za kisheria, ambao umewezesha kufanikisha kampeni hii kwa ufanisi.
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inaendelea kutekelezwa katika mikoa mingine, na matarajio ni kuwafikia wananchi zaidi, huku ikiimarisha amani, usawa, na haki katika jamii.
Matokeo ChanyA+ Chombo kinachounga mkono matokeo yote chanyA+ TanzaniA+. #InfoChanyA+