Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi mteule wa Tanzania nchini Japan Mhe. Anderson Mutatembwa, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma

Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amemsihi Balozi Mutatembwa kuzingatia kipaumbele cha nchi ambacho ni diplomasia ya uchumi kwa kuhakikisha anavutia wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nchini Japan pamoja na kuimarisha ushirikiano wa ubia.

Amemsisitiza Balozi Mutatembwa kuhakikisha makampuni ya Japan yanawekeza nchini Tanzania ili kuongeza thamani ya bidhaa hapa nchini na kuuza katika soko la Japan na soko la kimataifa. Amesema ni vema kushawishi wamiliki wa viwanda kuwekeza nchini Tanzania hususani viwanda vya magari, viwanda vya dawa na vifaa tiba pamoja na viwanda vya bidhaa za kielektroniki. Pia amesema kwa kuwa Japan inafanya vizuri katika sekta ya lojistiki ni vema kuvutia ushirikiano kwa kuzingatia kuwa Tanzania ni lango kwa mataifa mbalimbali.

Halikadhalika, Makamu wa Rais amemtaka Balozi Mutatembwa kuvutia uwekezaji katika sekta muhimu za kimkakati kama vile Utalii, Kilimo na Uvuvi pamoja na sekta ya Afya. Amesema nchi ya Japan ni wabobezi katika matibabu ya magonjwa yasiyoambukizia kama vile magonjwa moyo na figo hivyo ni vema kuendelea kutafuta fursa za masomo ya ubobezi kwa Watanzania.

Pia ametaka kusimamia utekelezaji wa vipengele vya Mpango wa Ushirikiano kati ya Japan na nchi za Afrika pamoja na kusimamia hati za makubaliano na ushirikiano zilizopo baina ya miji ya Tanzania na Japan.

Unaweza kuangalia pia

DAMU YA WATANZANIA NI YETU SOTE

Sote ni wamoja, Majonzi ya mmoja ni ya wote. Tanzania moja, haki na umoja. Tuwe …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *