Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, amefanya ziara maalum katika ofisi za ITV zilizopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam. Ziara hiyo ililenga kuimarisha ushirikiano kati ya Mamlaka na kituo hicho cha habari katika juhudi za kuhabarisha na kuelimisha umma juu ya tatizo la dawa za kulevya nchini.
Akiwasili katika makao makuu ya ITV/Radio One, Kamishna Jenerali Lyimo alipokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa ITV/Radio One, Bi Joyce Mhaville, pamoja na Mhariri Mkuu wa ITV, Bw. Steven Chuwa.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao walijadili njia za kuimarisha mahusiano ya kikazi na kuendeleza ushirikiano wa kimkakati, hususan katika kufikisha taarifa na elimu sahihi kwa wananchi kuhusu madhara ya dawa za kulevya na mbinu za kujikinga.
DCEA na ITV wamekubaliana kutumia vyema majukwaa ya habari na vipindi maalum kuhamasisha jamii, hususan vijana, ili kupunguza vitendo vinavyohusiana na matumizi na usambazaji wa dawa za kulevya.
Kwa hatua hii, ushirikiano wa taasisi hizi mbili unatarajiwa kuongeza ufanisi wa kampeni za kitaifa za kupambana na dawa za kulevya na kuimarisha uelewa wa umma katika kulinda afya na mustakabali wa taifa.
Kauli mbiu: kataa dawa za kulevya timiza malengo