Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) inashiriki kikamilifu katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika jijini Dodoma. Unapofika kwenye lango kuu la kuingilia viwanja vya maonesho, takribani mita 100 upande wa kushoto, utaliona banda la Ofisi ya Waziri Mkuu likiwa na maonyesho ya kipekee kutoka DCEA.
Karibu ulitembelee ujionee kwa macho aina mbalimbali za dawa za kulevya, ujifunze kuhusu madhara yake kiafya, kijamii na kiuchumi, na kufahamu hatua mbalimbali zinazochukuliwa na mamlaka katika mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya dawa hizo. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuteketeza mashamba ya kilimo haramu cha bangi na mirungi katika maeneo mbalimbali nchini na kuhamasisha kilimo cha mazao mbadala katika maeneo yaliyoteketezwa bangi na mirungi.
Kama hujawahi kuyaona, utapata nafasi ya kutambua mmea wa bangi, kujua muonekano wa heroini, skanka, na hata biskuti zilizotengenezwa kwa kutumia bangi. Haya yote yamewekwa kwa lengo la kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya madhara ya dawa za kulevya na jinsi ya kujikinga nayo.
Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo, Ndugu Aretas Lyimo, anakukaribisha kwa moyo mkunjufu kutembelea banda hili ujifunze zaidi kuhusu vita dhidi ya dawa za kulevya. Kataa dawa za kulevya, timiza malengo yako.