Kilimanjaro, Februari 17, 2026.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama hususan Jeshi la Polisi, kuanzia tarehe 10 hadi 16 Februari, 2026, imefanya operesheni maalum katika vijiji vya Marieni na Mhero vilivyopo kata ya Chome, wilaya ya Same, Kilimanjaro na kufanikiwa kukamata kilogramu 299.8 za dawa za kulevya aina ya mirungi pamoja na kuteketeza ekari 203 za mashamba ya mirungi. Watuhumiwa saba (07) wamekamatwa kuhusiana na uhalifu huo.
Pamoja na jitihada za Serikali za muda mrefu katika kutoa elimu, kufanya operesheni za mara kwa mara, kuimarisha miundombinu na kufikisha miradi ya maendeleo, bado kuna watu wachache wanaoendelea kukaidi sheria za nchi na kujihusisha na kilimo na biashara ya zao haramu la mirungi.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambaa na Dawa za Kulevya haitavumilia uhalifu huo na itaendelea kushirikiana na viongozi wa vijiji, kata, wilaya na mkoa pamoja na wadau wengine kutoa elimu pamoja na kufanya operesheni endelevu ili kuhakikisha tatizo la mirungi linadhibitiwa kikamilifu katika mkoa wa Kilimanjaro.
Wananchi wanaombwa kuendelea kushiriki katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa maendeleo endelevu ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Imetolewa na; Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
MAMLAKA YA KUDHIBITI NA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA.
Matokeo ChanyA+ Chombo kinachounga mkono matokeo yote chanyA+ TanzaniA+. #InfoChanyA+