Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo, ametangaza msamaha kwa wote watakaojisalimisha na kukiri kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, alipokuwa akiteketeza tani 4.402 za dawa za kulevya katika zoezi lililofanyika Oktoba 3, 2025, katika kiwanda cha saruji cha Twiga kilichopo Wazo, jijini Dar es Salaam.
“Tutatoa msamaha kwa wauzaji wa dawa za kulevya watakaoamua kukiri na kuacha. Hatutachukua hatua yoyote dhidi yao, bali tutashirikiana nao ili kufichua mbinu zinazotumika kuficha na kusambaza dawa hizi,” alisema Lyimo.
Kwa mujibu wa taarifa ya DCEA iliyosomwa na Kamishna Jenerali Aretas Lyimo, dawa zilizoteketezwa ni pamoja na kilo 2,168.18 za methamphetamine, kilo 1,064.29 za heroin, gramu 326.95 za cocaine, kilo 515.48 za bangi na kilo 653.74 za mirungi. Zote zilikuwa sehemu ya vielelezo vya mashauri mbalimbali yaliyopo mahakamani; baadhi yakiwa tayari yametolewa hukumu na mengine yakiendelea kusikilizwa.
Miongoni mwa mashauri yanayohusiana na dawa zilizoteketezwa ni kesi ya Najim Abdallah Mohamed iliyohusisha heroin kilogramu 882.71 na methamphetamine kilogramu 2,167.29. Aidha, mashauri yaliyotolewa hukumu ni Pamoja na ya Hassan Azizi aliyepatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha, Salum Shaaban Mpangula aliyehukumiwa kifungo cha maisha, Hemed Juma Mrisho maarufu kwa jina la “Hororo” aliyehukumiwa kifungo cha maisha, Ramadhan Shaban Gumbo aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, Irene Dickson Mseluka aliyehukumiwa miaka mitano jela na Gema Victor Mmasy aliyehukumiwa miaka mitatu jela.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema mamlaka itaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha vita dhidi ya dawa za kulevya inafanikiwa. Aidha, alisisitiza kuwa DCEA haitabaki katika hatua za kisheria pekee bali pia itatoa nafasi kwa wale wanaojihusisha na biashara hiyo kuachana nayo kwa hiari.
Matokeo ChanyA+ Chombo kinachounga mkono matokeo yote chanyA+ TanzaniA+. #InfoChanyA+