
Na Nuru Mwasampeta, WM
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ameutaka uongozi wa Mgodi wa Stamigold kuwajali wafanyakazi na kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuongeza uzalishaji katika mgodi huo. Amesema ,uongozi wa wizara utafika mgodini hapo mara kwa mara kusikiliza na kutatua changamoto zao ili kuongeza uzalishaji.
Amewataka viongozi hao kufanya kazi na wasambazaji na wataalamu wa nje wenye uadilifu na ufanisi mkubwa ili kusaidia katika kuongeza uzalishaji mgodini hapo. “Msione shida kuvunja mikataba na makampuni yasiyokwenda na kasi mnayoitaka katika kuzalisha dhahabu mgonini hapa,”Nyongo alisisitiza.
Nyongo alitoa kauli hiyo Aprili 13, 2020 alipotembelea Mgodi wa Serikali wa Stamigold unaosimamiwa na Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) na kukiri kuridhishwa na maendeleo ya uzalishaji mgodini hapo.
Amesema, tofauti na ilivyokuwa awali kwa mgodi huo, mwaka huu faida ya uzalishaji imeonekana kabla hata ya kumaliza mwaka ambapo faida ya uzalishaji imeongezeka kutoka shilingi billioni 2.7 mpaka kufikia shilingi billioni 5 na kuwa na mategemeo ya kuongezeka kwa faida mpaka bilioni kumi kwa mwaka ujao.

Kutokana na changamoto ya ugonjwa wa corona duniani, Naibu Waziri Nyongo amesema, bado bei ya dhahabu katika soko la dunia ipo juu na kuwataka watumishi katika mgodi huo kuhakikisha wanachukua taadhari za kujikinga na ugonjwa wa corona kama inavyoelekezwa na wataalamu wa afya huku wakiendelea kufanya kazi kwa juhudi.
Akizungumzia bei ya dhahabu katika soko la dunia, Nyongo amesema kuwa, bei ya wakia moja imepanda kutoka dola za kimarekani 1200 hadi dola 1500. “Kutokana na ongezeko hilo la bei ya dhahabu duniani Tanzania na Stamigold kama wazalishaji wa bidhaa hiyo tunapaswa kutumia fursa hiyo kuzalisha kwa wingi ili kupata faida kulingana na uhitaji wake kwa sasa,”Nyongo alisisitiza.
Waziri Nyongo alibainisha kuwa, kunapotokea majanga kama la corona nchi nyingi zinatunza fedha zao kwa mfumo wa dhahabu hivyo hununua na kuhifadhi dhahabu kutokana na ukweli kwamba thamani ya dhahabu huongezeka kadri siku zinavyoendelea.
Hivyo sekta ya madini ni sekta pekee yenye inayoonesha uwepo wa fursa hata katika msimu huu wa corona hivyo tuchukue tahadhari zote na kuendelea kuzalisha kwa bidii.
Aidha, ameushukuru uongozi wa mgodi huo kukubali maelekezo ya Serikali ya kuwataka kuuza dhahabu inayozalishwa mgodini hapo katika soko la ndani ambapo faida ya shilingi milioni 132 zimepatikana kutokana na uuzwaji wa dhahabu hiyo nchini.
Kwa upande wake Meneja wa Mgodi, Mhandisi Gilay Shamika amesema, utafiti uliofanywa na kampuni hiyo umeonesha uwepo wa wakia 71146 zitakazozalishwa kwa muda wa miaka mitano na wakati huo huo utafiti mwingine umeonesha kuwepo kwa wakia 106854 zitakazozalisha dhahabu kwa kipindi cha miaka saba na hivyo kufanya uhai wa mgodi kuwa wa miaka 12 kuanzia mwaka 2019/2020.