Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali italipa fidia kwa wananchi katika maeneo ambayo miradi ya Serikali imepita.
Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati akihutubia wakazi wa Manerumango kwenye uwanja wa shule ya msingi Maneromango wilayani Kisarawe mkoani Pwani.

“Nataka niwahakikishie wananchi wote kila kipande cha ardhi cha mtu kinachochukuliwa kwa ajili ya maendeleo ya Serikali au maendeleo ya Taifa basi kipande kile kitalipiwa fidia tutalipa fidia kwa viwango ambavyo sheria zetu zinaruhusu nataka niwaambie hakuna mtu atanyimwa haki yake, haki zote fidia zote zitalipwa kama inavyopaswa lakini huenda tukachelewa kwa sababu mambo ni mengi na rasilimali tuliyonayo inabidi tuigawe kwa vizuri zaidi” alisema Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais ameupongeza Uongozi na Wananchi wa Wilaya ya Kisarawe kwa kuja na Mpango wa Tokomeza Zero.
Aidha Makamu wa Rais alipokea msaada wa vifaa mbali mbali vya kituo cha afya Manerumango kutoka benki ya NMB vyenye thamani ya shilingi milioni 15.

Katika ziara yake leo, Makamu wa Rais alitembelea mradi wa ujenzi wa tenki la maji lenye ujazo wa lita milioni sita lililopo eneo la Mnarani, alikagua ujenzi wa barabara za lami Kisarawe mjini, pia alitembelea kiwanda cha saruji cha Lucky Cement.
Makamu wa Rais yupo kwenye ziara ya siku sita ya kukagua na kuhamasisha shughuli za kimaendeleo katika mkoa wa Pwani.

Mbunge wa Jimbo la Kisarawe ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo aliishukuru serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada zake za kuboresha miundo mbinu ya maji, umeme na barabara.