
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja, ameitaka Kampuni ya Andoya inayozalisha Umeme kwa kutumia Maporomoko ya Maji ya Mto Mtandazi kutanua wigo wa Kampuni hiyo ili kuongeza uzalishaji zaidi.
Masanja alisema hayo, Agosti 01, 2020, wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma,wakati wa ziara yake ya kutembelea mradi huo ili kuona shughuli za kufua na kuzalisha Umeme wa Megawati moja kwa kutumia Maporomoko ya Maji ya Mto Mtandazi zinazofanywa na kampuni hiyo tangu mwaka 2015.

Alisema kampuni ya Andoya inazalisha umeme ambao huliuzia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na pia katika Vijiji vitatu vilivyokaribu na mradi huo ambavyo ni Lifakara, Kilimani na Mbangamao.
Masanja aliueleza Uongozi wa Andoya kuwa wana uwezo na nafasi kubwa ya kuweza kutanua mradi huo na kuongeza uzalishaji wa Umeme kwakuwa eneo la mradi ni kubwa na linatosha.
“Kampuni yenu inanafasi kubwa ya kukuwa kiuzalishaji,sababu mnachanzo cha uhakika ambacho kina maji ya kutosha na yanayopatikana muda wote, azma ya Serikali ni kuwa na uwezo wa kuzalisha MWA 10,000 ifikapo 2025. hivyo, mchango wa wazalishaji wadogo unahitajika sana”, alisema Mhandisi Masanja.

Aidha alizitaka Taasisi za kifedha kuendelea kushirikiana na kuwaunga mkono wazalishaji binafsi wa umeme nchini kwa kuwapatia mikopo pale inapohitajika kwa lengo la kujenga, kuboresha au kutanua wigo wa mradi husika kwa kwakuwa miradi hiyo inadumu kwa muda mrefu.
Aliwasihi wasimamizi wa mradi huo waendelee kuusimamia vizuri ili uendelee kuzalisha umeme kwa kuwa miradi ya kuzalisha umeme wa maji ikisimamiwa vizuri huishi na kudumu kwa muda mrefu.

Vilevile aliwaagiza wasimamizi husika wa mradi huo kubadilisha Mita za umeme zinazotumiwa na wateja wao katika vijiji vitatu vilivyo karibu na mradi huo ambazo ni za mfumo wa kizamani zinazomruhuru mteja kutumia kwanza huduma ya umeme ndipo alipie, badala yake wawafungie mita za LUKU zinazotumika sasa ambazo mteja hulipia umeme kadri anavyotumia.
Aliendelea kusisitiza kuwa jukumu la Serikali ni kupitia Wizara ya Nishati ni kutunga Sera na kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji katika Sekta ya Nishati. Kwa muktadha huo, Wizara ya Nishati pamoja na Taasisi zake itaendelea kusimamia sheria, taratibu na kanuni za uwekezaji katika sekta ya Nishati ili kuendelea kuvutia wawekezaji nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Andoya, Alex Andoya aliishukuru serikali kupitia Wizara ya Nishati na Taasisi ziliochini yake kwa ushirikiano walioutoa kwa kampuni hiyo tangu kuanzishwa kwake hadi sasa.

Na Zuena Msuya, Ruvuma
Aidha aliahidi kushirikiana na taasisi za kifedha kuongeza uzalishaji wa umeme katika mradi wao kama alivyoshauriwa kwa kuwa wanachanzo cha uhakika cha kuzalisha umeme.
Aidha alieleza kwa ufupi juu ya mradi huo, kwa kueleza kuwa Ujenzi wa Mradi wa Andoya ulibuniwa na Marehemu Baba yake Mzee Mbunda Andoya ambapo ulijengwa kwa awamu mbili (2), ya kwanza ilihusu ujenzi wa mtambo wa kuzalisha MW 0.5 ambapo ujenzi ulianza mwaka 2013 na kukamilika mwaka 2015.
Awamu ya pili ilihusisha uwekaji wa mtambo wa MW 0.5 ambapo ulikamilika mwaka 2018 na kuwa na jumla ya mitambo yenye kuzalisha MW 1.0.